Kunenepa Kupita Kiasi Husababishwa na Nini?
“Tunakabili tatizo kubwa ambalo linaweza kuathiri sana afya ya watoto wetu. Hatua isipochukuliwa sasa ili kuzuia tatizo hilo, watu watazidi kunenepa kupita kiasi.”—William J. Klish, profesa wa magonjwa ya watoto.
WATU fulani wasio na tatizo la kunenepa huwachambua watu walionenepa kupita kiasi na kuwaona kuwa wavivu na goigoi. Lakini je, kweli tatizo hilo ni dogo hivyo? Je, kunenepa kupita kiasi ni tatizo la watu wavivu wasiopenda kufanya mazoezi? Au je, mara nyingi tatizo hilo husababishwa na mambo makubwa ambayo ni vigumu kuyazuia?
Je, Husababishwa na Urithi, Mazingira, au Yote Mawili?
Kitabu Food Fight kinasema hivi: “Kwa muda mrefu watu wamejadili ikiwa kunenepa kupita kiasi husababishwa na urithi au mazingira.” Ni nini maana ya urithi katika habari hii? Wengine husema kwamba kwa kawaida mwili wa mwanadamu huhifadhi kalori za ziada kwa ajili ya mahitaji ya wakati ujao. Kitabu hicho kinaendelea kusema: “Kwa makumi ya miaka, uchunguzi umefanywa ili kugundua jinsi urithi unavyosababisha kunenepa kupita kiasi. . . . Utafiti mwingi umefanywa kuhusu chembe za urithi za wanadamu na kunenepa kupita kiasi. Mbinu za hali ya juu zinatumiwa kutambua chembe za urithi zinazowafanya watu wawe na uwezekano wa kunenepa na kupata magonjwa kama vile kisukari. Kulingana na wanasayansi, yaelekea kwamba asilimia 25 hadi 40 ya uzito wa mwili hutegemea chembe za urithi.” Kitabu hicho kinasema hivi pia: “Ijapokuwa watu wanene kupita kiasi hulaumiwa kwa kujisababishia hali hiyo, idadi hizo zinaonyesha wazi kwamba chembe za urithi zinahusika sana, ingawaje, inasemekana kwamba mazingira huhusika kwa asilimia 60 au zaidi katika kuamua uzito wa watu.” Hilo linaonyesha kwamba mtindo wa maisha ya mtu ni kisababishi kikuu cha kunenepa kupita kiasi. Je, kila siku yeye hula vyakula vyenye kalori nyingi na kutumia kalori chache? Je, yeye hula vyakula visivyofaa? Je, yeye hutenga wakati kila siku ili kufanya mazoezi kwa kiasi?
Kliniki ya Mayo inaeleza kisababishi cha kunenepa kupita kiasi kwa maneno haya rahisi: “Huenda chembe za urithi zikasababisha kunenepa kupita kiasi, lakini uzito wa mwili hutegemea hasa kile unachokula na mazoezi ya mwili. Mwishowe, kula vyakula vyenye kalori nyingi kupita kiasi, kutofanya mazoezi, au yote mawili husababisha kunenepa kupita kiasi.” (Italiki ni zetu.) Kliniki hiyo inaendelea kusema hivi: “Haimaanishi kwamba ni lazima uwe mnene kwa sababu ya chembe za urithi. . . . Ingawa chembe zako za urithi zinahusika, uzito wa mwili hutegemea kile unachochagua kula na mazoezi unayofanya.”
Mashirika ya kuwasaidia watu kupunguza uzito hupata mamilioni ya dola kwani watu wengi hutamani sana kurudia umbo lao la zamani. Hata hivyo, wataalamu husema nini kuhusu kupunguza uzito? Kitabu Food Fight kinasema: “Ni vigumu sana kushughulikia tatizo la kunenepa kupita kiasi, na wengi wanaopunguza uzito huongeza uzito tena. Inakadiriwa kwamba ni asilimia 25 [robo moja] tu ya watu ambao hufaulu kupunguza uzito na kuudumisha, baada ya jitihada nyingi.”
Hatari za Kunenepa Kupita Kiasi
Kunenepa kupita kiasi kunaweza kusababisha matatizo makubwa ya afya. Dakt. Scott Loren-Selco, mtaalamu wa mfumo wa neva katika Kituo cha Tiba cha Chuo Kikuu cha Southern California, anaonya kwamba hata vijana walionenepa kupita kiasi wanakabili hatari ya kupata Aina ya 2 ya ugonjwa wa kisukari. (Ona Amkeni! la Mei 8, 2003.) Anasema hivi: “Tunaona wengi wakiugua ugonjwa huo siku hizi, na inaogopesha sana. Mimi huwaambia [watu walionenepa kupita kiasi] kwamba ninaweza kuwapeleka kwenye chumba cha wagonjwa wa kisukari ili niwaonyeshe madhara wanayoweza kupata: hiyo inatia ndani vipofu, watu waliokatwa miguu, na watu wengi sana ambao wamelemazwa kabisa na aina ya 2 [ya kisukari]—kwa sababu ya kunenepa kupita kiasi.” Ni nini husababisha hali hiyo? Loren-Selco anasema hivi: “Kwa sababu wana pesa, wao hununua mikate mikubwa iliyotiwa nyama katikati na chipsi. Hakuna anayewaonya kwamba kula vyakula vingi vya aina hiyo kutawafanya wanenepe kupita kiasi, iwe ni wenye biashara hizo za chakula, au madaktari ambao hawajafundishwa kuhusu lishe.”
Dakt. Edward Taub, mwandishi maarufu kuhusu lishe, anasema: “Hivi karibuni, watu wameamini kwamba kunenepa sana ni jambo la kawaida na linalokubalika maishani. Wazo hilo la ajabu linaendelezwa na wenye biashara za chakula ambao hupata faida kwa kutunenepesha.”
Wataalamu wanasema kwamba watu walio na mafuta mengi mapajani huenda wakawa na afya nzuri kuliko wale walio na mafuta mengi tumboni (hasa ikiwa kiuno chao kinazidi sentimeta 90 hadi 100). Kwa nini? Kitabu Mayo Clinic on Healthy Weight kinasema kwamba “kuwa na mafuta tumboni huongeza uwezekano wa kupanda kwa shinikizo la damu, kupata ugonjwa wa moyo, kisukari, kiharusi, na aina fulani za kansa. Ikiwa una nyonga kubwa, mapaja manene, na matako makubwa, basi hukabili hatari kubwa sana ya afya.”
Hivyo, mamilioni ya watu wazima na watoto ulimwenguni pote ambao wamenenepa kupita kiasi na wanakabili uwezekano wa kupata magonjwa hatari wanaweza kufanya nini? Je, kuna matibabu yanayofaa?
[Sanduku/Chati katika ukurasa wa 5]
BMI Ni Nini? Inaonyesha Nini?
BMI (body mass index) ni kipimo cha kulinganisha kimo na uzito ili kutambua ikiwa mtu ni mnene au mnene kupita kiasi. Kulingana na Kliniki ya Mayo, BMI ya 18.5 hadi 24.9 inaonyesha kwamba mtu ana afya bora. Ikiwa BMI yako ni kati ya 25 na 29.9, basi wewe ni mnene. Ikiwa imepita 30, basi wewe ni mnene kupita kiasi. Unaweza kutumiaje chati ya BMI? Je, unahitaji mashauri ya daktari ili upate madokezo au ujue hali yako?
Ili ujue BMI yako, gawa uzito wako katika kilo kwa kimo chako katika meta, kisha ugawe tena matokeo kwa kimo chako katika meta. Kwa mfano, ikiwa una kilo 90 na kimo cha meta 1.8, BMI yako ni 28 (90 ÷ 1.8 ÷ 1.8 = 28).
[Chati]
Mwenye Afya Mnene Mnene Kupita Kiasi
BMI 18.5-24.9 25-29.9 30 au zaidi
Kimo Uzito katika kilo
1.47 m 53 au chini 54-64 65 au zaidi
1.50 56 au chini 57-67 68 au zaidi
1.52 57 au chini 58-69 70 au zaidi
1.55 59 au chini 60-71 72 au zaidi
1.57 61 au chini 62-73 74 au zaidi
1.60 63 au chini 64-76 77 au zaidi
1.63 66 au chini 67-79 80 au zaidi
1.65 67 au chini 68-81 82 au zaidi
1.68 70 au chini 71-84 85 au zaidi
1.70 72 au chini 73-86 87 au zaidi
1.73 74 au chini 75-89 90 au zaidi
1.75 76 au chini 77-91 92 au zaidi
1.78 79 au chini 80-94 95 au zaidi
1.80 80 au chini 81-97 98 au zaidi
1.83 83 au chini 84-100 101 au zaidi
1.85 85 au chini 86-102 103 au zaidi
1.88 89 au chini 90-106 107 au zaidi
1.90 90 au chini 91-108 109 au zaidi
[Hisani]
Kwa mujibu wa Mayo Clinic on Healthy Weight
[Sanduku katika ukurasa wa 5]
Kalori ni nini?
Kalori ni nini? Ni kipimo cha nishati ya joto. Hivyo, unapotokwa na jasho unatumia kalori, au nishati ya joto. “Kalori ni kiasi cha joto kinachohitajiwa kuongeza halijoto ya kilo moja ya maji kwa sentigredi moja.” (Balance Your Body, Balance Your Life) Kila mtu huhitaji viwango tofauti-tofauti vya kalori au nishati kila siku, ikitegemea kimo, uzito, umri, na shughuli anazofanya.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 6]
Unahitaji kufanya mazoezi ikiwa
▪ Unatumia wakati mwingi kila siku ukiwa umeketi, iwe ni kutazama televisheni, kufanya kazi ofisini, au kusafiri ndani ya gari
▪ Mara nyingi hutembei kwa zaidi ya meta 100
▪ Unafanya kazi ambayo haikuwezeshi kufanya mazoezi
▪ Hutumii dakika 20 hadi 30 kufanya mazoezi angalau mara moja kila juma
Comments
Post a Comment