Kunenepa Kupita Kiasi Husababishwa na Nini?
“Tunakabili tatizo kubwa ambalo linaweza kuathiri sana afya ya watoto wetu. Hatua isipochukuliwa sasa ili kuzuia tatizo hilo, watu watazidi kunenepa kupita kiasi.”—William J. Klish, profesa wa magonjwa ya watoto. WATU fulani wasio na tatizo la kunenepa huwachambua watu walionenepa kupita kiasi na kuwaona kuwa wavivu na goigoi. Lakini je, kweli tatizo hilo ni dogo hivyo? Je, kunenepa kupita kiasi ni tatizo la watu wavivu wasiopenda kufanya mazoezi? Au je, mara nyingi tatizo hilo husababishwa na mambo makubwa ambayo ni vigumu kuyazuia? Je, Husababishwa na Urithi, Mazingira, au Yote Mawili? Kitabu Food Fight kinasema hivi: “Kwa muda mrefu watu wamejadili ikiwa kunenepa kupita kiasi husababishwa na urithi au mazingira.” Ni nini maana ya urithi katika habari hii? Wengine husema kwamba kwa kawaida mwili wa mwanadamu huhifadhi kalori za ziada kwa ajili ya mahitaji ya wakati ujao. Kitabu hicho kinaendelea kusema: “Kwa makumi ya miaka, uchunguzi umefanywa ili kugundua jinsi urit...