Dhehebu na Kanisa

Hili ni swali zuri kabisa ambalo inabidi tujiulize.Ikiwa dhehebu si kanisa, na kanisa si dhehebu, basi dhehebu ni kitu gani?

            Mimi mwenyewe nimekuwa nikijiuliza swali hili muhimu, tangu nilipofahamu maana halisi ya kanisa, kama neno la Mungu linavyotuambia. Mchungaji mmoja wa siku nyingi, aliwahi kuniambia kuwa madhehebu mbali mbali ya kikristo ulimwenguni ni viungo mbali mbali vya mwili wa Kristo.

            Ukiangalia jambo hili kijuu-juu tu, unaweza ukakubaliana na usemi wa mchungaji huyo. Lakini ukilichunguza jambo hili kwa “jicho” la Neno la Mungu utaona ya kwamba usemi huo si sahihi hata kidogo.

            Nilipousikia usemi huo kwa mara ya kwanza, ulinifanya nianze kuiangalia biblia kwa undani zaidi, ili niweze kupata ukweli wa maana ya kanisa na dhehebu, na uhusiano uliopo katikati yao.

            Nilianza na Neno kanisa, kwa kusoma na kutafakari kila mahali katika biblia palipoandikwa kanisa au makanisa. Na nikakuta ya kwamba neno kanisa au makanisa limetokea katika biblia kwa mara zisizopungua tisini na tisa. Na maana ya Kanisa ni mwili wa Kristo. (Waefeso 1:22,23) na mwili wa Kristo ni muunganiko wa roho za watu waliozaliwa mara ya pili kwa Roho wa Mungu popote walipo ulimwenguni (1Wakorintho 12:12-27; Warumi 12:4-21; Yohana 3:1-21, Matendo ya Mitume 2:37-47).

            Hakuna mahali ambapo nilikuta pameandikwa ndani ya biblia ya kuwa madhehebu ni viungo vya kanisa, au pameandikwa ya kuwa dhehebu ni kanisa au kanisa ni dhehebu. Kwa sababu hii, hamu yangu ilizidi sana ya kutaka kujua biblia inasema nini juu ya madhehebu.

            Kwa hiyo nilianza kusoma na kutafakari kila mahali katika biblia nilipokuta pameandikwa neno dhehebu au madhehebu. Na ninakuta ya kwamba neno dhehebu au madhehebu limetokea katika biblia kwa mara tano hivi.

            Na nilikuta ya kuwa madhehebu yalikuwepo hata KABLA ya Yesu Kristo kuzaliwa na bikira Maria, kama Mwana wa Mungu.

            Biblia inazungumza juu ya “Madhehebu ya masadukayo” (Matendo ya Mitume 15:5)

            Madhehebu haya yalikuwepo tangu kabla Yesu Kristo hajazaliwa duniani kama Mwana wa Mungu na Mwana wa Adamu. Na alipokuwa duniani katika maisha yake ya mwanzo alilelewa katika namna na jinsi madhehebu hayo yalivyokuwa yanamwabudu Mungu. Alitahiriwa siku ya nane kama ilivyokuwa desturi ya wayahudi na madhehebu hayo. Na wazazi wake wakamtolea sadaka kama ilivyokuwa desturi yao katika kufuata torati ya Musa (Luka 2:21-24)

            Madhehebu hayo ya Mafarisayo na Masadukayo yalikuwa yanamwamini Mungu wa Israeli, ambaye pia ni Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, na ni Baba yetu sisi. Na madhehebu ya kikristo yanamwamini Mungu huyo huyo.

            Lakini Yesu Kristo alipoanza kuhubiri juu ya habari njema za Ufalme wa Mbinguni uletao wokovu, walidhani analeta machafuko kati yao, wakamshitaki, wakamsulubisha na wakamuua. Lakini siku ya tatu akafufuka kutoka katika wafu, na mpaka leo yupo hai, akiwa ndiye tumaini letu la uzima wa sasa na wa baadaye.

            Ingawa madhehebu hayo yalikuwa yanamwamini Mungu mmoja na kutumia wote torati hiyo hiyo ya Musa, yalikuwa yanatofautiana katika mapokeo yao. Hebu soma na kutafakari habari hii:

“Paulo alipotambua ya kuwa sehemu moja ni Masadukayo, na sehemu ya pili ni Mafarisayo, akapaza sauti yake katika ile baraza, Ndugu zangu, mimi ni Farisayo, mwana wa Farisayo; Mimi ninahukumiwa kwa ajili ya tumaini la ufufuo wa wafu. Alipokwisha kunena hayo palikuwa na mashindino baina ya Mafarisayo na Masadukayo, mkutano ukafarakana. Kwa maana Masadukayo husema ya kwamba hakuna kiyama wala malaika wala roho; bali Mafarisayo hukiri yote.” (Matendo ya Mitume 23:6-8)

            Tunaona ya kuwa mkutano huu uliokusanyika ili kumhukumu Paulo, ulifarakana kwa sababu ya tofauti za mapokeo ya madhehebu yao. Hata hivi leo mahali pengi wakristo wamefarakana kwa sababu ya tofauti za mapokeo ya madhehebu yao. Hili ni jambo la kushangaza kwa sababu, madhehebu hayo ya kikristo, yote yanakiri kumhubiri Kristo, na kumwamini Mungu mmoja katika yeye.

            Lakini swali linajitokeza hapa nalo ni hili; Je! Kristo akihubiriwa huwa anawafarakanisha watu na kuwatawanya, au huwa anavuta WOTE kwake? Soma Yohana 12:32 imeandikwa:-

            “Nami (Yesu) nikiinuliwa juu ya nchi, nitawavuta wote kwangu.”

            Ikiwa ni hivyo basi, ni Yesu yupi anayehubiriwa siku hizi ambaye anatawanya watu?

            Ni kweli kwamba Neno la Mungu lililetwa na Yesu, linamwondoa mtu toka Ufalme wa giza na kumwingiza katika Ufalme wa Mungu (Wakolosai 1:13). Na pia neno la Mungu linamtenga mtu na tamaa za dunia.

            Lakini pia Neno lenye pumzi ya Mungu limewekwa ili kuwaunganisha watu wa aina mbali mbali pamoja na Mungu katika roho na kweli, kwa njia ya damu na ufufuo wa Yesu Kristo!

            Na nilipoendelea kuisoma, nilishangaa kuona kwamba biblia, haitumii maana ya neno dhehebu moja kwa moja na iliyo wazi kama vile ilivyofanya kwenye maana ya kanisa. Neno dhehebu limetumika katika misingi ambayo wasomaji wanatarijiwa wawe wanafahamu maana yake.

            Kwa hiyo niliposoma maana ya neno dhehebu kama ilivyotolewa na kamusi mbali mbali za maneno, niliona zimelieleza neno dhehebu sawa sawa na jinsi lilivyotumika katika biblia, na jinsi linavyotumika hivi leo.

            Dhehebu ni jamii ya watu waliokubaliana wao wenyewe kufuata utaratibu wa aina fulani katika kumwabudu Mungu, ambao wao wanauona ni bora zaidi kuliko wa dhehebu jingine. Hii ndiyo maana kila dhehebu linavutia kwake katika kuzungumza na watu juu ya kumwabudu Mungu.

            Na wadhehebu ya Kikristo ni mengi, na ya taratibu zinazotofautiana za kumwabudu Mungu. Na kila dhehebu linaona utaratibu wake wa kuabudu ni mzuri kuliko wa dhehebu jingine. Na kwa sababu hii kuna faraka kati ya wakristo wa madhehebu mbali mbali.

            Tangu siku nyingi sana ulimwengu kuna madhehebu ya aina mbali mbali. Kuna madhehebu ya kikristo, ya kiislamu, ya kihindi, na kadhalika. Madhehebu yote hayo yana taratibu zao za kumwabudu Mungu, ambazo zinatofautiana.

            Lakini namshukuru Mungu, kwa kuwa ukristo si dhehebu. Ukristo ni maisha ya Mungu yaliyodhihirishwa ndani ya Kristo, anayekaa ndani ya watu. Ukristo ni tabia ya Kristo. Mtu anakuwa mkristo, kwa kuwa anaonyesha tabia ya Kristo katika maisha yake, kwa kuongozwa na Roho wa Kristo.

            Ndiyo maana imeandikwa, “Lakini mtu awaye yote asipokuwa na Roho wa Kristo, huyo si wake”. (Warumi 8:9b)

            Wakristo wa kweli, walio na Roho wa Kristo, hao ndio Kanisa yaani mwili wa Kristo.

            Ukristo si dhehebu, na kanisa si dhehebu. Umoja wa kanisa si umoja wa madhehebu. Umoja wa kanisa upo na umoja wa madhehebu upo.

            Neno la Mungu linatuambia ya kuwa mwili wa Kristo ni mmoja (1Wakorintho 12:20). Kwa hiyo kanisa ni moja tu ulimwengu pote.

            Hakuna kanisa zaidi ya moja ambalo ni mwili wa Kristo. Lakini madhehebu ni mengi sana duniani.

            Je! bado una mawazo ya kuwa madhehebu ni viungo mbalimbali vya Kanisa? Watu wengi wana mawazo ya namna hii. Lakini biblia haisemi hivi:

            “Basi ninyi mmekuwa mwili wa Kristo na viungo kila kimoja peke yake.”

            Neno halisemi kuwa; “Basi madhehebu yamekuwa mwili wa Kristo ni viungo kila kimoja peke yake.”

            Neno linasema kuwa; “ Basi NINYI mmekuwa mwili wa Kristo na viungo kila kimoja peke yake.”

            Ni kweli kwamba kuna WATU walio viungo vya mwili wa Kristo walio ndani ya madhehebu mbali-mbali ya kikristo. Lakini madhehebu yenyewe si viungo vya mwili wa Kristo.

            Kwa nini naeleza haya?

            Ni kwa kuwa kama tusipofahamu tofauti na uhusiano uliopo kati ya kanisa na dhehebu; basi haitakuwa rahisi kwetu kufahamu sababu zilizomfanya Yesu Kristo atuombee umoja.

            Kwa sababu ya kutokufahamu uhusiano huo, watu wengi wamekuwa wakiomba juu ya umoja wa madhehebu WAKIDHANI wanaomba juu ya umoja wa kanisa. Na kwa sababu hii maombi hayo hayajajibiwa, kwa kuwa wanaomba umoja ili wautumie kwa tamaa zao. (Yakobo 4:1-3)

            Ni kweli pia kuwa katika siku za mwisho kutatokea umoja wa madhehebu kama ilivyotabiriwa. Lakini hatutalijadili suala hili katika somo hili.

            Lakini nina uhakika ya kwamba watu wengi wanataka na wanapenda kuwe na umoja katika mwili wa Kristo. NA NDILO LILILOKUWA LENGO LA KRISTO KATIKA KUTUOMBEA UMOJA.

            Na katika madhehebu ya Kikristo, kila moja limeanzishwa kwa kutumia mistari michache katika biblia. Na ili mtu aweze kuruhusiwa kushiriki katika dhehebu fulani ni sharti kwanza atimize masharti ya dhehebu hilo analotaka kuingia.

            Na kuingia katika mwili wa Kristo kuna masharti yake ambayo ni kuzaliwa upya mara ya pili na Roho Mtakatifu. (1Wakorintho 12:13, Yohana 3:5)

            Lakini katika madhehebu utakuta watu wa aina mbili kubwa; waliozaliwa mara ya pili kwa Roho wa Mungu na ambao bado hawajazaliwa mara ya pili kwa Roho Mungu.

            Yesu Kristo alipokuwa anaomba juu ya umoja alikuwa anaomba kwa ajili ya wale tu waliozaliwa mara ya pili kwa Roho wake na watakaozaliwa baadaye kabla ya yeye kurudi mara ya pili kulichukua kanisa.

            Ninapoyasema haya simaanishi ya kuwa uyachukie madhehebu, bali ufahamu tofauti iliyopo kati yake na kanisa. Na kwamba kukubaliwa na dhehebu fulani haitoshi kukurithisha ufalme wa Mungu, BILA ya kuzaliwa mara ya pili kwa Roho wa Mungu.

            BILA kumpokea Kristo moyoni mwako na kuwa mwana wa Mungu (Yohana 1:12) kuwa mkristo wa dhehebu tu hakutatosha kitu.

Hii ni kweli kabisa!

            Biblia inazungumzia juu ya “madhehebu ya Masadukayo” (Matendo ya Mitume 5:17) Na pia Biblia inazungumza juu “Madhehebu ya Mafarisayo” (Matendo ya Mitume 15:5)

            Hayo madhehebu yalikuwepo hata kabla ya Yesu kuzaliwa. Yesu Kristo alipotembea juu ya nchi alikutana nayo. Na fahamu ya kuwa viongozi wa madhehebu ndio waliomsulubisha Yesu Kristo.

            Sasa nauliza swali: Ikiwa Mungu aliona ya kuwa madhehebu yanatosha kumpatanisha yeye na mtu, kwa nini basi alimtuma Yesu Kristo, Mwana wake afe kwa ajili yetu?

            Mungu alikuwa na sababu muhimu kabisa. Mungu alijua kabisa kuwa taratibu za madhehebu haziwezi kuleta ondoleo la dhambi.

            Mungu alijua kabisa kuwa taratibu za madhehebu haziwezi kumpa mtu uzima wa milele.

            Kwa hiyo ilibidi Yesu Kristo aje azaliwe, afe na afufuke ili kila amwaminiye apate ondoleo la dhambi na uzima wa milele. (Yohana 3:16-18)

Comments

Popular posts from this blog

GROUP (KUNDI) ZA DAMU NA TABIA ZAKE

TOFAUTI YA DHAMBI,MAKOSA NA UOVU.

Madini ya Zink na Ugumba