SIKILIZA: CHANZO CHA SIKUKUU YA KRISMASI
Kila tunapokaribia sikukuu ya Krismasi, watu wengi wanauliza maswali juu ya chanzo cha Sherehe hii ya Krismasi ya tarehe 25 Desemba katika Ukristo, hivyo nimeona nitoe majibu ambayo naamini yatawasaidia wengi wanaopenda kuujua ukweli.
Maswali:
Ni nini Chanzo cha sikukuu ya Krismasi ya tarehe 25 Desemba? Je ni kweli Yesu alizaliwa tarehe hiyo? Ilianzaje na ilianza lini kusherekewa na Wakristo?
MaJibu:
Kwa mujibu wa Biblia, wakristo wengi wanaamini kuwa Yesu alizaliwa, ila hakuzaliwa tarehe 25 Desemba, na hakuna sehemu yoyote ya biblia inayotaja tarehe ya kuzaliwa Yesu, wanafunzi wa Yesu pamoja na Kanisa la Kristo waliloliacha mitume hawakuwahi kusherekea sikukuu hii ya Tarehe 25 Desemba kama siku ya Kuzaliwa Yesu Kristo.
Tunapochunguza Biblia tunaikuta tarehe 25 December, kuwa ni sikukuu iliyokuwa inaadhimishwa na wapagani wa Babeli ambako Waisraeli walichukuliwa mateka. Hivyo sikukuu ya 25 Desemba ilikuweko kabla ya Kuzaliwa Yesu, na ilikuwa sikukuu ya wapagani wa Babebli wakisherehekea kuzaliwa kwa Mtoto wa mungu JUA aliyeitwa TAMUZ.
Biblia inatoa historia au maelezo juu ya jambo hilo la kufanya sherehe ambayo mfalme wa wapagani aliitumia kufungua baadhi ya wafungwa, kama msamaha wakati wa sikukuu - Yeremia 52:31 “Hata ikawa, katika mwaka wa thelathini na saba wa kuhamishwa kwake Yehoyakini, mfalme wa Yuda, katika mwezi wa kumi na mbili, siku ya ishirini na tano ya mwezi, Evil-Merodaki, mfalme wa Babeli, katika mwaka wa kwanza wa kumiliki kwake, akamwinua kichwa chake Yehoyakini, mfalme wa Yuda, akamtoa gerezani.”
Nabii Yeremia aliandika kitabu hicho zamani kabla ya Yesu kuzaliwa, taifa la babeli lilikuwa na Desturi ya kuweka huru wafungwa katika siku hii ya Kuzaliwa kwa tamuz tarehe 25 Desemba. Enzi hizo haikuwa inaitwa Krismasi. Historia ya babeli kufanya Ibada ya Jua ni ya siku nyingi, na wengi wanaifahamu kama inavyoelezwa kwa ufupi hapa chini.
Kulikuwa na mfalme wa babeli aliyeitwa Nimrodi, na mke wake Nimrodi ambaye pia aliitwa Malkia wa Mfalme jina lake aliitwa semiramis, baada ya mfalme Nimrudi kufariki, mke wa mfalme akabeba mimba nje ya ndoa. Ili kuficha kitendo hicho cha mke wa mfalme kubeba mimba wakati mume wake amefariki, akatunga UONGO kuwa Mume wake HAKUFA ila alibadilika kuwa Jua (SUN), hivyo mionzi ya jua wanayoiona ndiyo iliyomdunga mimba. Wababeli kwa kuwa walikuwa waabudu mizimu waliamini Uongo huo na kuanza Kuliheshimu Jua (SUN) kama mungu wao.
Usiku wa kuamkia Tarehe 25 Desemba, Semiramis akazaa Mtoto aliyemwita TAMUZ, ambaye baba yake ni mungu Jua. Imani yao ilienda mbali zaidi hadi kuamini kuwa tendo la Semiramisi kuzaa na mungu jua yeye pia ni mungu mke na Mtoto wao Tamuz akaitwa mungu mwana. Kuanzia kipindi hicho wapagani wa Babeli waliiweka tarehe 25 mwezi wa 12, kuwa sherehe kubwa ya kuzaliwa kwa mungu mwana Tamuz.
SIKUKUU HII YA JUA ILIINGIAJE KATIKA UKRISTO?
Kwa kuwa Biblia haina maelezo yoyote juu ya wakristo kusherekea Sikukuu ya Krismasi, inabidi turudi kwenye historia ya Kanisa ambayo inaweza tu kuthibitishwa na Vitabu vya Kumbukumbu za Kanisa lililofanya mabadiliko hayo. Tutakumbuka kuwa Baada ya Yesu Kufufuka na kupaa kwenda Mbinguni, mitume walipata misukosuko mikubwa juu ya kupeleka Injili katika mataifa yaliyokuwa na Desturi za Ibada ya Kipagani – Moja ya Desturi za Ibada Kinzani ilikuwa Desturi ya Ibada za kipagani za Dola ya RUMI.
Kwa wasomi wazuri wa historia za anguko la Dola ya Kirumi na Historia ya Kanisa chini ya Mitume wa Yesu, ni wazi wanafahamu vita iliyokuwepo kati ya Desturi za Dini ya kipagani ya Rumi na Dini ya Kristo, ambayo ilisababisha Mitume na Wakristo wengi baadaye wateswe na Kuuwawa. Mitume na wakristo wengi wa mwanzo waliteswa na kuuwawa na dola ya RUMI, kwa ajili ya kupinga Desturi za Ibada za Kipangani kuingizwa katika Dini ya Mungu wa mbinguni.
Baada ya miaka mingi kupita karibia zaidi ya miaka 300 Mfalme Constatino wa Dola ya Kirumi aliyekuwa anaabudu JUA alimua kuwa Mkristo, lakini hakutaka kuacha Desturi za Ibada za kipagani na kuifanyia sherehe miungu yake. Hivyo akaamuru sherehe ya kuzaliwa mungu mwana, Tamuz, iendelee kusherehekewa ila wakristo waambiwe kuwa ni siku ya kuzaliwa Yesu Kristo.
Katika kipindi hicho cha mageuzi ya Rumi ikiwa katika mchakato wa kutafuta mwafaka kati ya wapagani na wakristo, ndipo kanisa la Rumi (Roman Catholic) lilianzishwa rasmi. Unaweza tu kusadikisha haya kutoka katika vitabu vya Kanisa la rumi, ambao walitunza kumbukumbu na ndio walihusika katika mabadiliko haya. Baadhi ya Vitabu ambavyo mimi nimevisoma na vinauzwa kwenye (book shop) za kanisa ni kama vifuatavyo.
Kitabu cha “BUSTANI YA KATEKESTA” UK. 73: nukuu inasema “Kwa kweli, hakuna anayejua tarehe ya kuzaliwa kwa Yesu. Tarehe 25 Desemba ilikuwa sikukuu kubwa kwa wapagani, walikuwa wakifanya ibada zao kwa mungu JUA”. Kwenye karne IV mwaka 336 baada ya Kristo, viongozi wa Kanisa walionelea, siku hiyo, washerekee kuzaliwa kwa Yesu MWANGA, NURU ya Ulimwengu. ....”
Kitabu cha “ZIJUE BARABARA SIKUKUU – NOELI – PASAKA” uk. 56’:
“Yafaa tupitie historia hiyo fupi. Katika siku za mwisho za Dola ya kipagani ya Kirumi, Ibada za kuabudu JUA zilikuwa zikifanyika sana. Mjini Roma dini ya Mithras, mungu – jua wa kiajemi, ilistawi sana. Kaisari Aureliani akajengesha hekalu la jua lisiloshindika, mnamo mwaka 274. Sikukuu kubwa ya mungu – jua, ilifanyika kila tarhe 25 Desemba.
Kitabu cha “The Compact History of Roman cathoric church” Page: 30, “That was only the first step. When Constantine became sole emperor in AD 324, he began to actively Support Christianity, seeing it as the new unifying force within the Roman Empire, replacing the Roman goods. Constantine built churches; passed laws honouring SUNDAY, Christmas, and other Christian holy days ... and was baptized on his deathbed in ad 337”.
Kwa upande wa Kanisa, historia inasema, ilikuwa ni mwaka 336AD, ndipo kanisa lilipoamua kwamba, badala ya kuwa na sikukuu ya kipagani mjini Roma, iliyojulikana kama “Natalis Solis Invincti” au The Birthday of the invincible/unconquered Sun, iliyosherekekewa tarehe 25 Desemba, sasa tarehe hiyo iwe si kwa kuzaliwa jua, bali iadhimishwe kuzaliwa mwana wa Mungu – Yesu Kristo. Kwa mara ya kwanza kanisa lilikuwa linaendesha Misa tu, lakini baadaye mtindo wa sherehe za kipagani zikashamiri zenye sura ambayo hadi leo zinaendelea – zikitawaliwa na Vinywaji (Vileo), Vyakula na starehe za kila namna.
Historia pia inaeleza kuwa katika kipindi hicho cha kuingiza MAPOKEO Kanisani, wakati Rumi ya kipagani inageuka kuwa Rumi ya Kikristo kwa mashariti ya wafalme kuingia na Desturi za Ibada zao zilizokuwa zinapingana na Desturi za Ibada au Maagizo ya Mungu, vilizuka VITA nyingine kati ya Wakristo waliosimamia Ukweli wa Biblia na Wakristo wa Rumi. Wakristo wengi waliosimamia ukweli, waliuwawa na kuteswa chini ya Uongozi wa Kanisa la Rumi.
MASWALI AMBAYO WAKRISTO WENGI WANAENDELEA KUJIULIZA:
1. Kwa nini Mungu hakuona haja ya kuwa na siku au tarehe ya kuadhimisha kuzaliwa kwa Yesu Kristo ili mitume na wakristo wa kwanza waiadhimishe?
2. Kwa nini Mitume na Kanisa la Kwanza waliyapinga Mapokeo hayo ya Desturi za Rumi, hadi zaidi ya miaka 300, walipokuja kushindwa kwa Mateso na Mauaji? Inawezekana mitume hawakuwa na Roho mtakatifu?
3. Kama kweli kuna haja ya kuadhimisha kuzaliwa kwa Yesu Kristo, kwa nini isiwekwe tarehe na mwezi mwingine badala ya tarehe 25 Desemba mapokeo ibada za miugu?
ZINGATIA:
Japo siku hizi wakristo wengi wameamua kufumba macho, na kutotaka kujua vyanzo vya Desturi za Mapokeo kuingizwa katika kanisa la Kristo, kwa maelezo na sababu nyingi nzuri zinazotolewa kuhalalisha Mapokeo – Bado tunapaswa kusimamia ukweli wa NENO la Mungu TU.
- YESU anapaswa kuzaliwa na kuwa hai ndani ya mioyo Yetu kila dakika tunayopewa kuwa hai, na tunaadhimisha kwa utukufu wa kuunganishwa naye kila siku.
- Wakati adui anaitumia siku hii ya sherehe ya Krismasi (25 Desemba) kuuhadaa ulimwengu, huku akiwafanya wengi kukidhi viwango vya UOVU, akiteka fikra hadi za wakristo FEKI, kwa miwashawasha ya Sherehe ... Wakristo wa Kweli wanapaswa kuzilinda nafsi zao, ili wasinaswe.
MUNGU AWABARIKI WOTE MNAPOENDELEA KUTAFAKARI JUU YA UKWELI HUU UNAOTUSAIDIA KUKUA KIROHO NA HATIMAYE KUFANYA MATENGENEZO.
Asante sana kwa mafundisho mazuri juu ya Christmas.
ReplyDelete